Kulaaniwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mkutano wa Umoja wa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i108566-kulaaniwa_utawala_wa_kizayuni_wa_israel_katika_mkutano_wa_umoja_wa_afrika
Viongozi wa nchi za Kiafrika waliokutana mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, wamelaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 19, 2024 04:47 UTC
  • Kulaaniwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mkutano wa Umoja wa Afrika

Viongozi wa nchi za Kiafrika waliokutana mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, wamelaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Katika mkutano wa Umoja wa Afrika wa Jumamosi  Februari 17, Moussa Faki, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, aliyataja mashambulizi ya Israel huko Gaza kuwa ni ukiukaji wa wazi kabisa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kuishutumu Israel kuwa  inaangamiza wakazi wa Gaza. Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema: "Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ni ushindi kwa nchi zote zinazounga mkono suala la Palestina. Tunaunga mkono msimamo wa Afrika Kusini na tunataka kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kukomeshwa vita huko Gaza."

Moussa Faki

Mohammad Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambaye alihutubia kikao cha Umoja wa Afrika, pia ametoa wito wa kutengwa Israel kimataifa na kuwekewa vikwazo kwa ukiukaji wake wa sheria za kimataifa.

Tarehe 11 na 12 Januari Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilifanya vikao viwili vya wazi  mjini The Hague huko Uholanzi kwa ajili ya kusikiliza mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kufanya jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza.

Kwa kuzingatia mashambulizi ya kikatili yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wakazi wa Gaza, mahakama hiyo iliutaka utawala huo kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya kimbari dhidi ya raia wasiokuwa na hatia na kuboresha hali ya kibinadamu ya eneo hilo. Hata hivyo maamuzi ya mahakama hiyo hayakujumuisha suala la kusimamisha vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Uungaji mkono wa viongozi wa ngazi za juu wa nchi za Kiafrika kwa watu wa Palestina katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika na hatua yao ya kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza vinaonesha jinsi nchi na wanasiasa huru wanavyoendelea kuchukizwa na uhalifu wa Wazayuni huko Palestina.

Hatua hiyo Umoja wa Afrika vilevile imeunga mkono msimamo wa serikali ya Afrika Kusini wa kuufungulia mashtaka utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Mahakama ya Kimataifa ya Hakki (ICJ)

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika umeonesha mshikamano wa nchi za bara hilo na wananchi wa Palestina na juhudi za nchi hizo za kutaka kurejeshwa amani na kuhitimisha vita huko Gaza.

Inatupasa kusema hapa kuwa, Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa  ambayo ilianzishwa tarehe 7 Oktoba 2023 na makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na ubaguzi na jinai za Israel, imepelekea kujitokeza makundi mawili ya nchi katika uwanja wa kimataifa. 

Kundi la kwanza ni nchi na tawala huru ambazo haziko tayari kuidhinisha jinai na uhalifu unaofanywa na Israel eneo la Magharibi mwa Asia, na zinatilia mkazo udharura wa kuhitimishwa haraka iwezekanavyo vitendo viovu vya utawala huo ghasibu. Nchi za kundi hili zinataka viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wafikishwe mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya kimbari na jinai za kivita huko Gaza, na zinawatambua maafisa wa utawala huo kuwa ndio wahusika wakuu wa matukio ya hivi sasa katika vita vya Gaza.

Kundi la pili ni la Marekani na waitifaki wa Kimagharibi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao wanaendelea kutoa misaada ya kifedha na kijeshi kwa utawala huo haramu, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma; na licha ya maandamano ya ndani katika miji mbalimbali ya nchi za Ulaya na Marekani, hawako tayari kusitisha misaada yao kwa utawala katili wa Tel Aviv.

Rais Joe Biden wa Marekani na chinjachinja wa Gaza, Benjamin Netanyahu

Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika unaonesha kuwa, nchi huru zinaendelea kufuatilia jinai za utawala wa Kizayuni katika taasisi za kimataifa, japokuwa inasikitisha kuona kwamba, taasisi hizo zinazodhibitiwa na Marekani na washirika wake, zimeshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuwatetea watu wa Palestina na haki zao.