Jul 09, 2016 07:40 UTC
  • Mapigano yaendelea kushuhudiwa Sudan Kusini

Baada ya siku moja ya mapigano ya umwagaji damu kati ya waungaji mkono na wapinzani wa Sudan Kusini katika mji mkuu Juba, kumeripotiwa kutokea ufyatualianaji risasi katika eneo lililopo jirani na ikulu ya Rais.

Hata hivyo hakuna taarifa zaidi zilizoripotiwa kuhusiana na ufyatualianaji risasi huo.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amewaagiza raia kuwa watulivu huku ufyatualianaji risasi ukiendelea katika mji mkuu huo.

Siku ya Alhamisi wanajeshi watano waliuawa na wapiganaji walio watiifu kwa makamu wa rais Riek Machar.

Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ukionyesha wasiwasi wake kuhusiana na mapigano hayo mampya huko Sudan Kusini.

Matukio hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, leo taifa hilo changa zaidi barani Afrika linaadhimisha miaka mitano ya uhuru wake. Hata hivyo sherehe rasmi zimefutwa kutokana na ukosefu wa fedha.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

Tags