Feb 27, 2024 07:27 UTC
  • Benin yasema iko tayari kutuma maelfu ya askari nchini Haiti

Nchi nyingine ya Kiafrika ya Benin imetangaza utayarifu wake wa kutuma maelfu ya askari wataoungana na Kikosi cha Kimataifa cha kulisaidia jeshi la Haiti kupambana na magenge ya uhalifu.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Benin imesema iko tayari kutuma askari 2,000 nchini Haiti kuungana na kikosi hicho cha kimataifa kitakachoongozwa na Kenya.

Limemnukuu Linder Thomas-Greenfield, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa akithibitisha habari ya Benin kuwa tayari kutuma askari wake Haiti, ingawaje shirika hilo haliwajanukuu maafisa wa serikali ya Benin katika ripoti yake, wakizungumzia kadhia hiyo.

Mwezi Oktoba 2023, Umoja wa Mataifa ulikubali ombi la Haiti la kutumwa askari wa kigeni nchini humo, kufuatia mgogoro wa kisiasa na kiusalama uliopelekea kuuawa watu zaidi 5,000, na kulazimisha wengine zaidi ya laki 3 kuhama makazi yao. 

Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya Mahakama ya Juu ya Kenya kutangaza kuwa, mpango wa serikali katika taifa hilo la Afrika Mashariki wa kuwatuma askari polisi nchini Haiti kuongoza kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa ni kinyume na katiba.

Utovu wa usalama nchini Haiti

Pamoja na uamuzi huo wa mahakama, lakini Rais William Ruto amesisitiza kuwa Kenya itatuma polisi elfu moja nchini Haiti kusaidia kurejesha usalama pamoja na kupambana na makundi ya watu wenye silaha. Uamuzi wa serikali ya Nairobi wa kutuma ujumbe wa polisi elfu moja huko Haiti umepingwa na baadhi ya wanasiasa wa Kenya wakiongozwa na kinara wa kambi ya upinzani, Raila Odinga, ambaye amesema kuwa mpango huo si kipaumbele cha Kenya.

Serikali ya mpito ya Haiti inatoa wito kwa jamii ya kimataifa kutuma kikosi chake kuwasaidia maafisa wake ambao wameonekana kuzidiwa na magenge ya wahalifu. 

 

Tags