Mar 27, 2024 02:07 UTC
  • Kadhaa waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Liberia

Watu kadhaa wameripotiwa kufariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko kusini mwa Liberia.

Waziri wa Madini wa Liberia, Wilmot Paye jana Jumanne alithibitisha habari ya kutokea ajali hiyo na kuongeza kuwa, takwimu za awali zinaonesha kuwa watu wasiopungua saba wameaga dunia kwenye mkasa huo uliotokea usiku wa kuamkia jana.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, huenda idadi hiyo ikaongezeka, na kwamba tayari timu ya maafisa wa serikali imetumwa katika eneo la tukio katika Kaunti ya River Cess.

Paye amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha mkasa huo unaendelea, akisistiza kuwa serikali itaiwajibisha na kuibebesha dhima kampuni iliyokuwa inaendeleza uchimbaji wa madini katika eneo hilo kinyume cha sheria.

Shirika la habari la Reuters limenukuu mashuhuda na duru za habari zinazosema, makumi ya wachimba migodi  wamepoteza maisha katika ajali hiyo.

Uchimbaji madini

Nchi ya Liberia ambayo inapatikana magharibi mwa bara Afrika ina utajiri mkubwa wa madini kama vile dhahabu, almasi, chuma na mkaa wa mawe.

Hata hivyo shughuli za uchimbaji madini katika aghalabu ya matimbo ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika zinafanyika kinyume cha sheria na bila ya uangalizi wa vyombo vya dola.

Aghalabu ya madini hususan ya dhahabu yanayochimbwa kinyume cha sheria nchini humo pamoja na nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.