Apr 04, 2024 11:38 UTC

Masheikh wawili maarufu wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamezungumzia umuhimu wa Siku ya Kimataifa ya Quds na uungaji mkono wa Waislamu wa nchi hiyo kwa kadhia nzima ya Palestina hususan Ghaza.

Sheikh Musa Ahmad, mmoja wa viongozi wa Kiislamu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Iran Press kuhusu Siku ya Kimataifa ya Quds kwamba, Waislamu barani Afrika ni waungaji mkono wa kadhia ya Palestina na wataendelea kuwa na msimamo huo hadi watu wa Palestina wakomboe haki zao. 

Kwa upande wake, Sheikh Siru Ahmad, ambaye pia ni katika masheikh maarufu wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameliambia shirika hilo la habari la Iran Press kwamba, Waislamu wa mashariki mwa DRC wataungana bega kwa bega na Waislamu wengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Waislamu Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds

 

Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo kwa mwaka huu wa 2024 inasadifiana na Ijumaa ya kesho ya Aprili 5, itaadhimishwa kwa sura ya kipekee mwaka huu kutokana na jinai zinazoendelea kufanywa na Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa zaidi ya miezi sita sasa huko Ghaza Palestina.

Ubunifu wa Imam Khomeini, MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds imeyabakisha hai mapambano ya haki ya ukombozi wa Palestina kiasi kwamba Siku ya Quds inazidi kupata umaarufu duniani, mwaka baada ya mwaka.

Pamoja na mambo mengine, Waislamu hushiriki kwenye maandamano makubwa ya Siku ya Quds katika kona zote za dunia katika Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani kila mwaka ili kutangaza uungaji mkono wao kwa Kibla chao cha Kwanza yaani Msikiti wa al Aqsa na suala zima la Palestina.  

Tags