Ufaransa kuondoa askari wake Jamhuri ya Afrika ya Kati
Rais Francois Hollande wa Ufaransa ametangaza kuwa nchi yake itaondoa askari wake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza Jumatano mjini Paris, Hollande amesema Waziri wa Ulinzi Jean-Yves Le Drian ataenda Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Oktoba kutangaza rasmi kumalizika oparesheni za askari wa Ufaransa nchini humo maarufu kama Sangaris.
Oparesheni hiyo ilianzishwa Desemba mwaka 2013 kwa lengo la kusitisha machafuko yaliyokuwa yamejiri katika nchi hiyo baada ya kundi la magaidi wa Kikristo wajulikanao kama Anti Balaka kuwashambulia Waislamu ambapo maelfu waliuawa na wengine nusu milioni kulazimika kukimbia makazi yao.
Kikosi hicho kilichokuwa na askari 2,000 kililaumiwa kwa kutowasaidia Waislamu kwani hata pamoja na kuwepo kwao nchini humo Waislamu waliendelea kuuawa na kufurushwa kutoka makazi yao.
Halikadhalika askari wa Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamehusishwa na kashfa za ngono na udhalilishaji kijinsia wa watoto wadogo katika nchi hiyo.