Jun 15, 2024 10:55 UTC
  • Mahakama ya Niger yaondoa kinga ya kutoshtakiwa kwa Mohamed Bazoum

Mahakama ya juu ya Niger imeondoa kinga ya kutoshtakiiwa rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum, na hivyo kutoa fursa ya uwezekano wa kufunguliwa mashtaka dhidi yake.

Kulingana na rais wa mahakama hiyo, iliyoundwa mwezi Novemba mwaka jana na utawala mpya wa kijeshi, Abdou Dan Galadima, mahakama hiyo imeamuru kuondolewa kwa kinga ya kutoshtakiwa Bazoum, aliyepinduliwa mwezi Julai 2023.

Mamlaka ya Niger inamtuhumu Bazoum kwa uhaini, kufadhili ugaidi na kupanga njama ya kuhujumu serikali.  Amekuwa akizuiliwa kwenye makao ya rais kwenye mji mkuu Niamey tangu alipoondolewa madarkani Julai 26.

Kundi la mawakili wanaomwakilisha Bazoum limesema uamuzi huo unadhirisha ukiukwaji mkubwa wa haki nchini Niger.

Maafisa kadhaa wa Jeshi la Niger Julai mwaka jana walitangaza kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo.

Kanali Amadou Abdramane, aliyeandamana na maafisa wengine tisa, alisema vikosi vya ulinzi na usalama vimeamua kumpindua Bazoum kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na utawala mbaya.

Bazoum, ambaye ni mshirika wa karibu wa Ufaransa, alichaguliwa kuwa rais katika uchaguzi wa 2021 ambao ulikuwa wa kwanza wa mpito wa mamlaka ya kidemokrasia katika nchi hiyo ambayo imeshuhudia mapinduzi manne ya kijeshi tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo 1960.

Mkutano wa dharura wa ECOWAS ulioitishwa kujadili madhara ya mapinduzi ya kijeshi nchini Niger, uliamua kusitisha misaada yote ya kifedha kwa serikali ya Niamey, kusitisha shughuli za kibiashara, marufuku ya safiri kwa waliohusika na mapinduzi hayo, na kufunga mipaka na nchi hiyo.