Jun 16, 2024 02:36 UTC
  • Tunisia yawaondolea visa watalii kutoka Iran

Serikali ya Tunisia imeruhusu kuingia bila ya visa watalii wa Iran kuanzia jana Jumamosi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetangaza msamaha wa visa kwa wamiliki wa pasi za kawaida za Iran kwa madhumuni ya utalii.

Msamaha huo unaruhusu kukaa ndani ya ardhi ya Tunisia hadi siku 15 ndani ya kipindi cha siku 180. Msafiri lakini lazima aoneshe nafasi halali ya hoteli atakayofikia na tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi.

Sehemu moja ya taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ilisema katika taarifa yake ya juzi Ijumaa kwamba: Wamiliki wa pasipoti za kawaida wa Iran wataondolewa visa ya kuingia Tunisia kuanzia Juni 15 (yaani jana Jumamosi).

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imesema imechukua uamuzi huo wa kuwaondolea visa watalii kutoka Iran ikiwa ni kujibu wema kama huo ambao umefanywa na Iran kwa watalii kutoka Tunisia.

Tags