Jun 22, 2024 06:49 UTC
  • Musalia Mudavadi
    Musalia Mudavadi

Kinara wa Mawaziri wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema Muswada wa Fedha 2024 lazima upitishwe na kutiwa saini na Rais William Ruto kuwa sheria, akisema kinyume na hivyo itakuwa ni sawa na kuangusha Serikali.

Bw Mudavadi alisema hayo mjini Kabarnet, Baringo ya Kati, jana Ijumaa, wakati wa hafla ya kuchangisha pesa kusaidia vikundi vya kina mama, na kuongeza kuwa serikali haiwezi kuendeshwa bila ushuru na madeni.

“Muswada wa Fedha lazima upite kwa sababu ukiangushwa ni sawa na kuangusha Serikali. Kwa hivyo haya maandamano hayafai kupuuzwa kwa sababu wanachosema wanamaanisha kwamba wanataka kuangusha Serikali,” amesisitiza Mudvadi.

Alkhamisi iliyopita, wabunge 204 wa Bunge la Kenya walipiga kura kupasisha muswada huo ambao unapingwa vikali na idadi kubwa ya wananchi hasa vijana, katika hatua iliyomaanisha kwamba, unaingia katika “Committee Stage” ambapo mapendekezo ya kuondoa baadhi ya ushuru yatapigiwa kura. 

Bunge la Kenya

Waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana na chipukizi, wanataka muswada huo utupiliwe mbali, wala sio kukarabatiwa, wakisema kwamba licha ya mapendekezo ya kuondoa baadhi ya ushuru, bado kuna ushuru kwenye vipengele vingine ambao utafanya maisha kuwa magumu kuliko yalivyo sasa.

Tags