Tunisia yatangaza tarehe ya uchaguzi wa rais
Tume ya Uchaguzi nchini Tunisia imetangaza Oktoba 6 mwaka huu kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Mamlaka Huru ya Juu ya Uchaguzi Tunisia (ISIE) imetangaza hayo na kuongeza kuwa, itatoa orodha ya mwisho ya wagombea wa kiti cha rais mnamo Septemba 3. Shirika la habari la Tunis Afrique Presse (TAP) limenukuu taarifa ya mamlaka hiyo ikisema kuwa, kampeni za uchaguzi huo zitaanza Septemba 14 na kumalizika Oktoba 4.
Mamlaka Huru ya Juu ya Uchaguzi Tunisia imeongeza kuwa, matokeo ya mwisho ya uchaguzi ujao wa rais yatatangazwa kufikia Novemba 9. Tunisia hufanya uchaguzi wa rais kila baada ya miaka mitano.
Rais wa sasa Kais Saied ambaye aliingia madarakani mwaka 2019, na ambaye Julai 25, 2021 alichukua hatua za kipekee, ikiwa ni pamoja na kuizulu serikali ya Waziri Mkuu wakati huo, Hichem Mechichi, kulivunja Bunge na Baraza Kuu la Mahakama, na pia kuibadilisha katiba ya nchi na kutwaa madaraka yote ya nchi, hajatangaza iwapo atagombea muhula wa pili katika uchaguzi huo wa Oktoba au la.

Haya yanajiri wiki chache baada ya wafuasi wa chama cha Salvation Front wanaompinga Rais Kais Saied kuandamana katika mji mkuu Tunis, wakitaka kusafishwa mazingira na hali ya kisiasa, kupangwa tarehe ya uchaguzi wa rais, na kutoa dhamana ya uchaguzi wa kidemokrasia na wa haki kwa wananchi.
Vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika vimeonya kuhusu ushindani usio wa haki katika uchaguzi ujao wa rais. Vinakosoa mbinyo dhidi ya kila kiongozi na shakhsia ambaye ana nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo wa urais.