UNICEF: Watoto elfu 49 wanakabiliwa na utapiamlo Nigeria
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuwa, watoto 49,000 wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa na utapiamlo nchini Nigeria.
Manuel Fontaine, Mkurugenzi wa UNICEF katika eneo la Magharibi mwa Afrika amesema kwa jinsi mambo yalivyo hivi sasa na iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, karibuni hivi, kwa wastani watoto 134 wataanza kufariki dunia kila siku kutokana na utapiamlo, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Amezitaka nchi wafadhili kujitokeza katika kufanikisha mpango wa kuyanusuru maisha ya watoto hao na haswa watoto robo milioni ambao wanakabiliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu katika eneo la Borno, ambalo lilikuwa ngome ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.
Siku chache zilizopita, Yemi Osinbajo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Nigeria alisema watu milioni 110 wanaishi katika umaskini wa kupindukia nchini humo, idadi ambayo ni asilimia 80 ya wananchi wote wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta. Alisema kuwa, nchi yake inahitajia dola bilioni 2.5 kuweza kumaliza kikamilifu ukata nchini humo na kuongeza kuwa, umaskini ndiyo changamoto kuu inayoikabili serikali ya hivi sasa ya nchi hiyo.