Leseni ya al-Arabiya kufanya kazi nchini Algeria yafutiliwa mbali
(last modified 2024-10-21T07:28:32+00:00 )
Oct 21, 2024 07:28 UTC
  • Leseni ya al-Arabiya kufanya kazi nchini Algeria yafutiliwa mbali

Viongozi wa Algeria wameamua kufutilia mbali leseni ya mtandao na televisheni ya al-Arabiya ya Saudi Arabia nchini humo kwa kupotosha habari na kutoheshimu sheria na maadili ya taaluma ya uandishi na upashaji habari.

Shirika rasmi la habari la Algeria limeinukuu Wizara ya Mawasiliano ya nchi hiyo ikisema kuwa imeamua kufutilia mbali leseni ya kanali ya al-Arabiya nchini humo kutokana na ukiukaji wake wa wazi wa sheria za nchi hiyo kuhusu vyombo vya habari.

Televisheni ya al-Arabiya imekuwa ikigonga vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni katika nchi kadhaa za Kiarabu ikiwemo Iraq, kwa sababu za kichochezi, hasa kwa kuwataja viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina na Lebanon wanaojitolea muhanga kupigana na utawala ghasibu wa Israel kuwa ni magaidi.

Kufuatia uchochezi huo, vijana wa Iraq walivamia na kuchoma ofisi za televisheni hiyo mjini Baghdad na kutaka ofisi hizo zifungwe kabisa na kutoruhusiwa kufanya kazi nchini humo.