Jul 24, 2016 07:51 UTC
  • Wapinzani: Kuna njama ya kujaza nafasi ya Machar Sudan Kusini

Wafuasi wa karibu wa Riek Machar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini wamedai kuwa Rais Salva Kiir anapanga njama ya kujaza nafasi ya Machar ambaye kwa sasa hayuko katika mji mkuu Juba.

Nyarji Roman, msemaji na mpambe wa Machar amesema Rais Salva Kiir anapanga kujaza nafasi ya Makamu wa Rais na Taban Deng Gai, mmoja wa mawaziri wa upande wa Machar ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kuegemea upande wa Kiir. Roman amesema tayari Machar amempiga kalamu nyekundu waziri huyo, kwa kushiriki mazungumzo na Salva Kiir pasina idhini yake. Msemaji huyo wa Machar amesema Makamu wa Rais wa Sudan Kusini amemfuta kazi Taban Deng, Waziri wa Madini sambamba na kumtimua kwenye chama.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

 

Haya yanajiri siku chache baada ya Machar kukataa kuheshimu makataa ya masaa 48 aliyopewa na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo awe amerejea katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba kufikia Ijumaa iliyopita. James Gatdet Dak, mpambe wa Machar amesema makamu huyo wa rais hatorejea Juba hadi pale kikosi cha tatu cha jumuiya ya kieneo ya IGAD kitakapotumwa nchini humo kudhibiti hali ya mambo.

Wananchi wakimbia mapigano Juba

 

Machafuko mapya mjini Juba yaliibuka tarehe saba mwezi huu ambapo hadi sasa watu zaidi ya 300 wameripotiwa kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kulazimika kukimbia nchi. Kadhalika machafuko hayo yameathiri makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka jana 2015 kati ya mahasimu hao wawili.

Tags