RSF: Waandishi 54 wameuawa mwaka huu wakiwa kazini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120066-rsf_waandishi_54_wameuawa_mwaka_huu_wakiwa_kazini
Shirika la kimataifa la Waandishi Habari wasiokuwa na Mipaka, RSF limetangaza kuwa, takribani waandishi habari 54 wameuawa ulimwenguni kote mwaka huu katika mazingira yanayohusisha kazi zao.
(last modified 2024-12-13T00:08:47+00:00 )
Dec 13, 2024 00:08 UTC
  • RSF: Waandishi 54 wameuawa mwaka huu wakiwa kazini

Shirika la kimataifa la Waandishi Habari wasiokuwa na Mipaka, RSF limetangaza kuwa, takribani waandishi habari 54 wameuawa ulimwenguni kote mwaka huu katika mazingira yanayohusisha kazi zao.

Ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo iliyotolewa jana, imeeleza kuwa theluthi moja ya waandishi hao wameuawa katika Ukanda wa Gaza.

Sehemu nyingine yya ripoti ya RSF imesema hadi sasa idadi ya waandishi habari waliouawa, kulingana na takwimu za mwishoni mwa mwezi Novemba, ziko sawa na kiwango cha mwaka uliopita.

Shirika hilo limesema kuripoti kuhusu vita ni hatari sana, na kwamba waandishi habari 31 kati ya 54 waliuawa katika maeneo yenye mizozo.

Kulingana na RSF, idadi hiyo ni kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano.

Shirika la kimataifa la Waandishi Habari wasiokuwa na Mipaka limekuwa likiitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ikiwezekana iyachunguze mauaji ya wafanyakazi wa vyombo vya habari kama uhalifu wa kivita.

Hata hivyo hivi karibuni, Shirikisho la Kimataifa la Wanahabari (IFJ) lilitangaza kuwa 2024 umekuwa mwaka wa "mauti zaidi" kwa waandishi wa habari kutokana na waandishi 104 wa habari kuuawa duniani kote, huku zaidi ya nusu kati yao wakiuawa katika Ukanda wa Gaza.