Wananchi wa Sudan Kusini wanataabika na mafuriko
Mafuriko ya msimu yaliyoiathiri Sudan Kusini, ambayo hapo huko nyuma yalikuwa yanatabirika na yalikuwa ni sehemu ya maisha ya watu wa maeneo hayo, sasa yamekuwa janga la kila mwaka, na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa watu zaidi ya 379,000 wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na mafuriko yaliyoiathiri Sudan Kusini mwaka huu.
Sudan Kusini ambayo imetajwa na Benki ya Dunia kama nchi iliyo katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, haina suhula na vifaa vya kushughulikia athari za mafuriko.

Serikali ya Sudan Kusini haina uwezo wa kushughulikia majanga kama vile mafuriko, ambayo yanaendelea kuzamisha vijiji, kuharibu mashamba na kuua mifugo nchini humo. Zote hizo ni katika taathira mbaya za vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeeleza kuwa karibu jamii zote zilizoathiriwa na mafuriko katika kaunti ya Ayod huko Sudan Kusini zimekatikiwa na njia na hazina mawasiliano na ulimwengu wa nje. Barabara hazipitiki na zoezi la usambaji chakula linapasa kufanyika kwa njia ya ndege.
Hii ni katika hali ambayo Sudan Kusini inaendelea kutatizwa na matatizo ya kiuchumi kufuatia kuharibika bomba la mafuta katika nchi jirani ya Sudan na hivyo kukwamisha uuzaji nje mafuta.
Matatizo ya kiuchumi ya Sudan Kusini yamezidi kuwa mabaya kwani bomba la mafuta lililoharibika katika nchi jirani ya Sudan, lililosababishwa na vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe, limetatiza mauzo ya nje.