Rais wa Somalia aitembelea Ethiopia kwa mara ya kwanza tangu kupatiwa ufumbuzi mzozo wa nchi mbili
Ethiopia na Somalia zimekubali kurejesha na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili kupitia uwakilishi kamili wa kidiplomasia katika miji mikuu yao. Mataifa hayo mawili yalieleza haya katika taarifa ya pamoja jana Jumamosi.
Maafikiano haya yamefanyika baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kumlaki vyema Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia ambapo viongozi hao walizungumza kuhusu namna ya kuimarisha uhusiano na kupatia ufumbuzi kadhia muhimu za pande mbili.
Mwezi Aprili mwaka jana, Somalia ilimfukuza balozi wa Ethiopia nchini humo kufuatia mzozo wa bandari ya Somaliland na kufunga ubalozi mdogo wa Ethiopia huko Hargeisa hadi pale mzozo huo ulipopatiwa ufumbuzi kupitia azimio la Ankara.
Katika mazungumzo hayo ya Addis Ababa, Rais wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia wamesisitiza umuhimu wa jumbe zao za kidiplomasia kushirikiana kwa karibu katika makongamano ya pande kadhaa na ya kikanda kuhusu masuala ya maslahi ya pamoja.