25 wauawa katika machafuko ya kabla ya uchaguzi Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12160-25_wauawa_katika_machafuko_ya_kabla_ya_uchaguzi_afrika_kusini
Watu wasiopungua 25 wameuawa katika machafuko ya kabla ya uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Afrika Kusini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 28, 2016 15:30 UTC
  • 25 wauawa katika machafuko ya kabla ya uchaguzi Afrika Kusini

Watu wasiopungua 25 wameuawa katika machafuko ya kabla ya uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Afrika Kusini.

Duru za kiusalama zimearifu kuwa, mauaji hayo ya kisiasa yameshadidi hususan katika mji wa Pretoria na mkoa wa KwaZulu-Natal, ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Nkosinathi Nhleko, Waziri wa Masuala ya Jeshi la Polisi wa nchi hiyo amesema watu zaidi ya 13 wameuawa katika mkoa wa KwaZulu Natal katika kipindi cha siku chache zilizopita na kwamba watuhumiwa 23 wa mauaji hao wanashikiliwa na vyombo vya usalama. Habari zaidi zinasema kuwa, akthari ya waliouawa katika mkoa huo ni wafuasi wa chama tawala ANC. Mwanasiasa aliyeuawa hivi karibuni ni Nceba Dywilli, aliyekuwa akiwania uwakilishi wa mji wa Nelson Mandela Bay, mkoa wa Eastern Cape. Mauaji mengine ya hivi karibuni yanayoaminika kuwa ya kisiasa ni ya Tsietsi Mothibe na Kenny Monjomani wa chama cha Economic Freedom Fighters kinachoongozwa na kinara wa upinzani Julius Malema.

Maandamano ya wananchi dhidi ya serikali mjini Pretoria, Afrika Kusini

Tayari Wizara ya Masuala ya Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini imebuni jopo la wabunge la kuchunguza mauaji hayo sambamba na kuhakikisha kuwa, uchaguzi huo wa mabaraza ya miji unaotazamiwa kufanyika Jumatano ijayo unakuwa huru na wa haki na unafanyika chini ya anga ya utulivu na uthabiti.