Kiir: Nafasi ya Machar ilijazwa na SPLM yenyewe, sio mimi
Serikali ya Sudan Kusini imepuuzlilia mbali onyo la Umoja wa Mataifa kuhusu uteuzi wa viongozi wa kisiasa nchini humo na haswa uteuzi wa Makamu wa Rais mpya aliyechukua nafasi ya Riek Machar.
Samuel Makuei, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amekanusha taarifa kuwa Rais Salva Kiir ndiye aliyemteua Taban Deng Gai kujaza nafasi ya Riek Machar na kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, uteuzi huo ulifanywa na chama chenyewe cha upinzani cha SPLM.
Haya yanajiri siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kumuonya Rais Salva Kiir kuhusu uteuzi wa kisiasa unaofanyika katika kipindi cha sasa cha kushtadi mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq alisema kuwa uteuzi wa aina yoyote wa viongozi wa kisiasa huko Sudan Kusini unapaswa kuoana na makubaliano ya amani yaliyofikiwa yapata miaka miwili iliyopita kati ya pande hasimu nchini humo kwa shabaha ya kuhitimisha vita vya ndani.
Machar aliukimbia mji wa Juba baada ya kushadidi mapigano kati ya wafuasi wake na vikosi vya jeshi la serikali mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai. Hii ni katika hali ambayo, Sudan Kusini imekanusha tetesi kwamba kiongozi huyo wa upinzani ameuawa na kusisitiza kuwa, madai hayo ni propaganda zinazoenezwa na wafuasi wa Machar.
Machafuko mapya mjini Juba yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 300 hadi sasa na kutishia kuzuka tena vita vya ndani huko Sudan Kusini.