Jeshi la Somalia laangamizi magaidi 130 wa al-Shabaab kusini mwa nchi
(last modified Fri, 21 Feb 2025 06:51:18 GMT )
Feb 21, 2025 06:51 UTC
  • Jeshi la Somalia laangamizi magaidi 130 wa al-Shabaab kusini mwa nchi

Somalia imesema jeshi la nchi hiyo likishirikiana na vikosi washirika vimefanikiwa kuzima mashambulizi ya al-Shabaab, na kuua makumi ya wanachama wa genge hilo la kigaidi.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kuinukuu serikali Somalia ikisema jana Alkhamisi kwamba, wanajeshi wake pamoja na wanamgambo wa koo waoiunga mkono serikali wamepambana na uvamizi ulioratibiwa dhidi ya vijiji na kundi la kigaidi la al Shabaab kusini mwa nchi hiyo, na kuua zaidi ya washambuliaji 130.

Habari zaidi zinasema kuwa, jeshi pamoja na vikosi vya ndani vimeendelea kufanya operesheni kubwa katika maeneo tofauti ya Somalia kwa lengo la kulitokomeza kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.

Kundi hilo la wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda limefanya uasi wa umwagaji damu kusini na katikati mwa Somalia tangu mwaka 2007, na kuua maelfu ya watu katika kampeni ambayo imekumbwa na mashambulizi mabaya ya mabomu katika mji mkuu Mogadishu.

Haya yanajiri wiki moja baada ya makumi ya wanamgambo wa ISIS kuuawa katika makabiliano makali na vikosi vya usalama katika eneo linalojitawala la Puntland huko Somalia, huku vikosi vya usalama vikipata hasara pia katika mapigano hayo.

Nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi sasa, huku genge la al-Shabaab na makundi ya kigaidi ya Daesh (ISIS) yakiwa tishio kuu kwa usalama wa nchi hiyo.