Al-Shabaab yaendelea kumwaga damu za Waislamu Ramadhani
(last modified Wed, 12 Mar 2025 07:11:32 GMT )
Mar 12, 2025 07:11 UTC
  • Al-Shabaab yaendelea kumwaga damu za Waislamu Ramadhani

Wanachama waliokuwa wamejizatiti kwa silaha wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wamewauwa watu wasiopungua saba katika shambulio dhidi ya hoteli moja katika mji wa kati wa Somalia; ambapo wazee wa eneo hilo na maafisa wa serikali walikuwa wamekutana kujadili jinsi ya kuchukua hatua dhidi ya genge hilo la wanamgambo.

Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limetangaza kuhusika na shambulio hilo huko Beledweyne na kueleza kuwa, limewaua zaidi ya watu 10.

Shirika la habari la Reuters limeandika habari hiyo na kuongeza kuwa, magaidi hao waliingia kwa nguvu na kutumia mabavu kwenye mkahawa huo mjini Beledweyne, katikati mwa Somalia.

"Waliingia kwa nguvu na kuanza kuripua mabomu kwenye lango la hoteli," amesema mmoja wa mashuhuda wa shambulio hilo, muuza duka Ali Suleiman.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, vikosi vya jeshi la Somalia vikishirikiana na vikosi vingine vya ndani viliwaua wanamgambo wapatao 70 wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab katika operesheni ya mashambulizi viliyotekeleza katika maeneo kadhaa ya jimbo la Hirshabelle Kusini, katikati ya nchi hiyo.

Wanamgambo wa al-Shabaab

Operesheni hiyo ilikuwa ya kujibu mapigo kwa mashambulizi yaliyofanywa na  al-Shabaab katika eneo hilo mnamo siku chache kabla ya hapo.

Kundi la kigaidi la Al-Shabaab ambalo lina uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda limekuwa likipambana na serikali ya shirikisho ya Somalia kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Kundi hilo limefanya mashambulizi mengi ya mabomu na mengine katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine kadhaa ya nchi hiyo tete ya Pembe ya Afrika.