Somalia pia yapinga pendekezo la US kuhusu Wapalestina wa Gaza
Serikali ya Somali imepinga vikali pendekezo la Marekani la kuwapa makazi Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza kwenye ardhi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ahmed Moallim Fiqi amenukuliwa akisema, Somali haitaafiki pendekezo lolote linalokiuka haki ya Wapalestina kuishi kwa amani katika nchi yao.
Mbali na kukanusha madai kuwa Somalia imepokea ombi rasmi kutoka kwa Marekani juu ya suala hilo, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Somalia amesisitiza kuwa, "Hatutaunga mkono mpango wowote wa kuwapokea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi ya Somalia."
Awali, maafisa wa serikali ya Sudan walisema walikataa pendekezo hilo la Marekani, huku maafisa kutoka Somalia na Somaliland wakikana kuwepo mawasiliano ya aina yoyote kuhusiana na suala hili.

Afisa mmoja wa serikali ya Khartoum amenukuliwa akisema kuwa, serikali ya Donald Trump iliahidi msaada wa kijeshi kwa serikali ya Sudan dhidi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ujenzi mpya wa baada ya vita, na motisha zingine.
Washington na Tel Aviv ziliwasiliana na maafisa katika nchi tatu za Afrika Mashariki kujadili suala la kutumia maeneo ya nchi hizo kuwapa makazi Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.
Associated Press imenukuu duru za habari zikisema kuwa, mawasiliano yamefanywa na maafisa kutoka Sudan, Somalia, na eneo lililojitenga la Somaliland kuhusiana na pendekezo hilo.