RSF yaua raia 45 Al-Malha; jeshi la Sudan lasonga mbele
Zaidi ya raia 45 wameuawa katika shambulio la Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika eneo la Al-Malha, yapata kilomita 210 kaskazini mwa El Fasher, magharibi mwa Sudan.
"Leo (jana Jumamosi), wapiganaji wa RSF walianza tena vitendo vyao (hujuma) katika masoko na vitongoji vya makazi (katika eneo la Al-Malha)... na ufyatuaji risasi kiholela kutoka kwa RSF imesababisha mauaji ya zaidi ya raia 45," chanzo kutoka kwa Kamati za Uratibu wa Upinzani huko El Fasher kiliiambia Xinhua kwa sharti la kutotajwa jina.
Wakati huo huo, Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema kwenye mtandao wa X kwamba, RSF imefanya "mauaji makubwa" ya watu 48 katika eneo la Al-Malha, huku wengine 63 wakijeruhiwa wakati wa shambulio hilo. Jumuiya hiyo imeonya kwamba, "mauaji ya halaiki na ya kikabila" yanayofanywa na RSF dhidi ya wakazi wa Darfur yatapelekea hali kuwa ngumu zaidi katika eneo hilo.
Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) hakijatoa taarifa yoyote kufikia sasa kuhusiana na shambulio hilo la jana lililoua makumi ya raia huko Al-Malha, magharibi mwa Sudan.

Haya yanajiri huku Jeshi la Sudan jana Jumamosi likiendeleza ushindi wake kwa kuitwaa tena Benki Kuu na maeneo kadhaa ya kimkakati, na majengo ya serikali katikati mwa Khartoum, yakiwemo pia makao makuu ya Mkuu wa Ujasusi.
Juzi Ijumaa, jeshi la Sudan lilidhibiti tena ikulu ya rais katika mji mkuu Khartoum ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu vita vilipoanza kati ya jeshi la serikali SAF na RSF karibu miaka miwili iliyopita.
.