Kupanuliwa uhusiano wa Iran na Afrika ni changamoto kwa madola ya Magharibi
(last modified Wed, 30 Apr 2025 02:29:51 GMT )
Apr 30, 2025 02:29 UTC
  • Kupanuliwa uhusiano wa Iran na Afrika ni changamoto kwa madola ya Magharibi

Mkutano wa tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika ulifanyika mjini Tehran wakati kivuli kizito cha sera za nchi za Magharibi dhidi ya Iran na Afrika kimeathiri mahusiano mengi ya kimataifa kati ya Iran na Afrika.

Kuhusiana na suala hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesisitiza kuwa, chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) na propaganda chafu za madola ya Magharibi dhidi ya Afrika na kutaka Afrika ikimbiwe ni changamoto mbili muhimu katika kustawisha uhusiano wa Iran na Afrika ambayo inachochewa na nchi za Magharibi na akasema: Mkakati wa kustawisha uhusiano na ushirikiano wa dhati katika ngazi za juu na katika sekta zote na nchi za Kiafrika uko katika ajenda ya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mohamed Reza Aref sanjari na kubainisha kuwa nchi za Magharibi zinaendeleza chuki ya Iran kwa lengo mahususi na zinajaribu kuonyesha taswira isiyo ya kweli kuhusu Iran duniani kwa kuibua masuala ya uongo, alisema: Kwa kuongezeka uhusiano kati ya Iran na nchi nyingi za Kiafrika, vitisho visivyo na mantiki vilivyotokana na kuendelezwa na nchi za Magharibi sera ya chuki dhidi ya Iran vimeondolewa.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran aidha ameashiria kuwa, nchi za Magharibi zinaiona Afrika kuwa ni uwanja wa kujifaragua wa Wamagharibi ambao daima unapaswa kuwa kwa ajili ya madola hayo na hivyo kutaka kutumia rasilimali za bara hilo kongwe kama watakavyo. Makamu wa Rais wa Iran amesema bayana kwamba, kwa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano, tutaweza kuondoa stratijia hii isiyo ya kimaadili na isiyo ya kibinadamu."

Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika umefanyika katika katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni, bara la Afrika limekuwa moja ya vituo muhimu vinavyoweza kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na hata kijiografia duniani.

Idadi kubwa ya watu wa bara la Afrika, rasilimali nyingi na madini kama vile almasi, dhahabu, metali adimu, bidhaa kama vile kahawa na kakao, na rasilimali za mafuta na gesi, viimeyafanya mataifa ya dunia kulizingatia bara hilo na yanajaribu kupanua uhusiano wao na nchi za bara hili.

Hii ni katika hali ambayo, kwa kupanua sera ya kuuonyesha taswira mbaya kwa Afrika, Marekani na Magharibi zimeangazia matatizo ya nchi za bara hili na kuzionyesha kuwa ni nchi dhaifu na zisizo na ustaarabu. Rais wa Marekani Donald Trump pia amefuata sera hii mara kwa mara katika hotuba zake na amejaribu kuidhalilisha Afrika na kupanua sera za kuichafua Afrika.

Kwa upande mwingine, nchi za Magharibi zimekuwa zikiendeleza siasa za chuki dhidi ya Iran kwa miaka mingi sambamba na maslahi yao na zinajaribu kuzuia nchi mbalimbali hususan za Kiafrika zisiwe na uhusiano mzuri na Tehran. Propaganda za vyombo vya habari, upotoshaji wa ukweli, na kuonyesha taswira ya Iran isiyo na usalama na uthabiti ni sehemu ya fumbo hili tata la kisiasa.

Rais Masoud Pezeshkian akihutubia mkutano wa tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika mjini Tehran

Kuhusiana na suala hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutambua umuhimu unaoongezeka wa bara la Afrika, inajaribu kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa na nchi za bara hili, na kufanyika Kongamano la tatu la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika ni hatua moja mbele kuelekea katika lengo hilo.

Akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alizungumzia uwezo wa bara la Afrika na ulazima wa kuwepo ushirikiano na kueleza kuwa, Iran iko tayari kuzishirikisha nchi za Afrika mafanikio yake katika nyanja mbalimbali.

Iran hivi sasa inajaribu kupanua uhusiano wake na nchi za Kiafrika katika kiwango cha kistratijia kwa kuelewa ipasavyo hali ya sasa. Kwa hakika, kwa kupanua ushirikiano wa pande zote, Iran na Afrika zinaweza kuboresha hali katika sekta mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Katika muktadha huu, Iran inaweza kuchukua nafasi muhimu katika maendeleo ya nchi za Kiafrika kwa kusafirisha nje huduma za kiufundi na kiuhandisi na kujenga miundombinu muhimu kama vile mitambo ya kuzalisha umeme, mitambo ya kusafisha mafuta, mabwawa, barabara na mifumo ya mawasiliano ya simu.

Kwa upande mwingine, kuagiza malighafi adimu, nishati na mazao ya kilimo ya hali ya juu kutoka katika  nchi za Kiafrika nako kunaweza kukidhi baadhi ya mahitaji ya kiuchumi ya Iran. Hii ni pamoja na kuwa, maingiliano haya ya pande mbili yataleta mizani ya nguvu dhidi ya sera za ukiritimba za nchi za Magharibi.

Pia, kuimarisha misimamo ya pamoja katika taasisi za kimataifa kunaweza kuwa moja ya mhimili muhimu wa ushirikiano wa kisiasa.

Mkutano wa tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika Tehran 2025

Iran na nchi za Kiafrika zinaweza kuwakilisha sauti ya umoja katika majukwaa kama vile ya Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa kuchukua misimamo mimoja katika masuala kama vile ukoloni mamboleo, vikwazo vya upande mmoja, uingiliaji kati wa nchi za nje na haki za binadamu.

Mielekeo hii ya pamoja inaweza kuongeza uzito wa kisiasa wa nchi zinazoendelea na kupunguza umimi na ubabe uliopo katika mfumo wa kimataifa.

Ijapokuwa nchi za Magharibi bado zinataka sera ya makabiliano na Iran na kuidhalilisha Afrika ili iendeleze ubabe wake, na katika uga huu, zinahofia uhusiano wowote huru na wa kiubunifu kati ya Tehran na Afrika; lakini inaonekana kwamba hatua kama vile kufanya Kongamano la Kiuchumi la Iran na Afrika ni kikwazo kwa sera za nchi za Magharibi za kutengwa mataifa mengine na jukwaa la ushirikiano mkubwa unaozingatia kuheshimiana, maslahi ya pamoja, na mustakabali sawa kwa maslahi ya pande mbili.