Afrika Kusini yaanza kuchunguza jinai za enzi za 'apartheid'
(last modified Sat, 31 May 2025 10:45:01 GMT )
May 31, 2025 10:45 UTC
  • Afrika Kusini yaanza kuchunguza jinai za enzi za 'apartheid'

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amemteua Jaji mstaafu wa Mahakama ya Kikatiba, Sisi Khampepe kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC) ya kuchunguza ucheleweshaji wa mashtaka na uchunguzi wa jinai zilizofanyika enzi za ubaguzi wa rangi (apartheid) nchini humo.

Khampepe atasaidiwa na Jaji Mwandamizi mstaafu, Frans Diale Kgomo na wakili mtajika, Andrea Gabriel. Tume hiyo itashughulikia na kuchunguza matukio ya kibaguzi yaliyofanyika kuanzia mwaka 2003 hadi sasa.

Ramaphosa amesaini tangazo la kuundwa kwa tume hiyo ya kimahakama ya uchunguzi, ili kubaini iwapo majaribio yalifanywa kuzuia uchunguzi na kufunguliwa mashtaka kwa washukiwa wa uhalifu enzi za ubaguzi wa rangi.

Katika taarifa ya ofisi ya rais, kuanzishwa kwa tume ya uchunguzi ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa katika majadiliano ya suluhu kwenye shauri la mahakama, lililoletwa na familia za waathiriwa wa uhalifu uliofanyika enzi za apartheid.

Ramaphosa amesema: "Kwa miaka mingi, kumekuwa na madai ya kuingiliwa kwa kesi hizi. Uingiliaji huu unaodaiwa unaonekana kuwa sababu ya ucheleweshaji usiokubalika wa upelelezi na mashtaka ya uhalifu wa kikatili uliofanywa chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Hii imezisababisha familia za wahanga, uchungu na mfadhaiko.

CIA ilihusika katika kukamatwa Nelson Mandela

Duru mbali mbali duniani zimekuwa zikisisitiza kuwa, Marekani haistahiki kujipiga kifua na kudai kuwa kinara wa kutetea na kulinda haki za binadamu duniani kutokana na rekodi yake nyeusi, ikiwemo ya kuunga mkono mfumo wa 'apartheid' nchini Afrika Kusini.

Inaarifiwa kuwa, "Kuna wakati Marekani iliunga mkono utawala wa 'apartheid' nchini Afrika Kusini, na (Shirika la Ujasusi la Marekani) CIA lilihusika katika kukamatwa (Nelson) Mandela, aliyekuwa kiongozi wa mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini."