Kiir akataa azimio la kutumwa askari 4,000 zaidi Sudan Kusini
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amekataa azimio lililopasishwa Ijumaa iliyopita na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutumwa askari 4,000 zaidi wa kigeni nchini humo.
Akuei Bona Malwal, Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa amesema serikali ya Juba imepinga azimio hilo kwa kuwa lilipasishwa kwa haraka na bila kuzingatiwa hali halisi ya mambo nchini humo na matakwa ya serikali ya Rais Salva Kiir. Amesema ingekuwa vyema iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lingeshauriana na Sudan Kusini kabla ya kupasisha kwa jazba rasimu ya azimio hilo iliyoandaliwa na Marekani. Misri, Venezuela, Russia na China zilikataa kuunga mkono rasimu ya azimio hilo zikisema kuwa, askari hao watatumwa nchini Sudan Kusini bila ridhaa ya serikali ya Juba.
Taarifa iliyotolewa Ijumaa na serikali ya Juba muda mfupi baada ya Baraza la Usalama kupasisha pendekezo hilo la serikali ya Washington ilisema kuwa, hatua hiyo itashadidisha maradufu mgogoro wa nchi hiyo. Mapigano mapya nchini Sudan Kusini ambayo hadi sasa yamepelekea watu zaidi ya 300 kuuawa yanaendelea licha ya uwepo wa askari 12,000 wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa UNMISS katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Hatua ya Juba kukataa kuafiki azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inatazamiwa kuandaa mazingira ya kupitishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini.
Hii ni katika halia ambayo, iliarifiwa kuwa serikali ya Sudan Kusini mnamo Agosti 5 ilikubali pendekezo la jumuiya ya kieneo ya IGAD la kutumwa askari wa kulinda amani nchini humo, katika mkutano wa dharura wa wakuu wa jumuiya hiyo mjini Addis Ababa Ethiopia.