Mkuu wa WHO ataka hatua za haraka dhidi ya Ebola
Mwishoni mwa Mkutano wa 79 wa Baraza la Afya Duniani, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Matiafa la Afya Duniani (WHO) amezitaka nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kimataifa dhidi ya milipuko ya magonjwa hatari, akionya kuhusu tishio linaloongezeka la Ebola, virusi vya Hanta na majanga ya magonjwa yajayo.
Akizungumza na Mawaziri, wanadiplomasia na wataalamu wa afya mjini Geneva, Uswisi mwishoni mwa mkutano huo wa wiki nzima uliomalizika Jumamosi, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa milipuko ya hivi karibuni ya Ebola na virusi vya Hanta inaonesha kuwa dunia bado iko katika hatari ya magonjwa ya kuambukiza yanayosambaa kwa kasi.
Wito wake umetolewa wakati Uganda imethibitisha Jumamosi wagonjwa wapya watatu wa Ebola wa virusi aina ya Bundibugyo ambavyo hadi sasa havina tiba wala chanjo.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Dkt. Tedros amesema kuwa wagonjwa hao ni pamoja na mhudumu wa afya kutoka Uganda, dereva mmoja na raia mmoja wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) aliyesafiri kutoka Jimbo la Ituri kwenda Uganda kupata matibabu.
Amepongeza Wizara ya Afya ya Uganda kwa juhudi zake za kugundua, kufuatilia na kuwahudumia watu wanaoshukiwa au kuthibitishwa kuambukizwa Ebola. Amesema katika kipindi hiki muhimu cha kukabiliana na mlipuko huo, ni lazima mamlaka kuendelea kuwa makini ili kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
Mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola uliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini DRC Jumamosi iliyopita kabla ya visa kuripotiwa pia Uganda.
Ijumaa, WHO iliongeza kiwango cha tathmini ya hatari ya taifa kwa DRC hadi “juu sana”, ingawa hatari ya kimataifa bado imeendelea kuwa “ndogo”.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO pia amezitaka nchi wanachama kuendelea kuongeza michango yao ya kifedha ili kuhakikisha WHO inaendelea kuwa taasisi imara, huru na yenye uwezo wa kukabiliana na dharura za afya duniani siku zijazo.