Serikali ya DRC yasitisha safari za ndege Bunia kufuatia mlipuko wa Ebola
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imechukua hatua ya dharura kwa kusitisha safari zote za ndege zinazoingia na kutoka mjini Bunia, mashariki mwa nchi hiyo, ikiwa ni juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa hatari wa Ebola.
Uamuzi huo uliotangazwa na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano, umepiga marufuku shughuli zote za usafiri wa anga katika mji huo ambao ni makao makuu ya jimbo la Ituri, ambapo virusi hivyo vimezidi kushika kasi. Hata hivyo, kwa kuzingatia dharura za kitabibu, serikali ya Kinshasa imetoa idhini ya kipekee kwa safari za kibinadamu, ndege za matibabu, na zile za dharura, mradi tu zipate kibali maalum kutoka kwa mamlaka za anga na zile za afya.
Lengo la ruhusa hizo maalum ni kuhakikisha kuwa huduma muhimu hazikwami, hususan usafirishaji wa wataalamu wa afya, dawa, na misaada ya kibinadamu ambayo ni nguzo kuu katika kukabiliana na janga hili.
Hali ya mashariki mwa DRC inazidi kuwa tete kufuatia nchi jirani ya Uganda, ambayo ni lango kuu la biashara na mienendo ya watu kwa wakazi wa Bunia, kuweka vikwazo vya usafiri. Hatua hiyo imechukuliwa na serikali ya Kampala kama kinga ya kuzuia maambukizi ya Ebola kuvuka mpaka.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde kutoka Wizara ya Afya ya DRC, kufikia tarehe 26 Mei, 2026, ugonjwa huo umeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 220. Aidha, visa zaidi ya 930 vimeripotiwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, na Ituri.
Katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na baa hili, Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kimeeleza kuwa takriban dola milioni 500 zimeahidiwa na serikali mbalimbali za Afrika pamoja na washirika wa kimataifa. Fedha hizo zinalenga kusaidia mapambano dhidi ya Ebola nchini DRC na Uganda, pamoja na nchi nyingine zilizo katika hatari ya kukumbwa na mlipuko huo.
Wataalamu wa afya wamebainisha kuwa aina ya virusi vya Ebola vinavyosambaa sasa, vijulikanavyo kama Bundibugyo strain, ni miongoni mwa aina sita hatari zaidi za virusi hivyo, vikiwa na uwezo wa kuua hadi asilimia 50 ya watu wanaoambukizwa.