Operesheni za jeshi la Somalia na AMISOM dhidi ya ash-Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13948-operesheni_za_jeshi_la_somalia_na_amisom_dhidi_ya_ash_shabab
Jeshi la serikali ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa Umoja wa Afrika AMISOM, limetekeleza operesheni kubwa dhidi ya kundi la ash-Shabab kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2016 02:39 UTC
  • Operesheni za jeshi la Somalia na AMISOM dhidi ya ash-Shabab

Jeshi la serikali ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa Umoja wa Afrika AMISOM, limetekeleza operesheni kubwa dhidi ya kundi la ash-Shabab kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti, operesheni za askari hao zilizofanyika siku ya Jumanne iliyopita katika eneo la Bay, kwa akali zilipelekea wanachama wanane wa genge hilo la kigaidi kuangamizwa. Polisi ya Somalia imesema kuwa, Hassan Ganey, mmoja wa viongozi wandamizi wa ash-Shabab ni miongoni mwa magaidi waliouawa na kwamba hakukuwa na madhara yoyote kwa upande wa askari wa serikali au wale wa AMISOM. Shambulio la siku ya Jumanne lilitekelezwa katika hali ambayo siku ya Jumatatu Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisifu mafanikio ya operesheni za askari wa Somalia na AMISOM katika vita vyao dhidi ya wanachama wa kundi la ash-Shabab. Rais Kenyatta aliyasema hayo jijini Nairobi alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry ambapo sanjari na kuashiria juu ya mpango wa kuondoka kwa hatua askari wa AMISOM kutoka Somalia miaka miwili ijayo, alisema kuwa, suala muhimu lililosalia hivi sasa ni kuliwezesha jeshi la taifa hilo kusimamia usalama wa nchi baada ya kuondoka askari wa AMISOM.

Askari wa AMISOM akiwa katika operesheni dhidi ya magaidi wa ash-Shabab, Somalia

Hata hivyo pamoja na juhudi hizo, lakini wanachama wa genge la ash-Shabab bado wameendeleza mashambulizi ya kigaidi nchini humo. Kwa akali watu 15 waliuawa na kujeruhiwa siku ya Jumapili katika miripuko miwili ya mabomu katikati mwa Somalia. Mohamed Abdi Fani, mmoja wa makamanda wa polisi wa Somalia amenukuliwa akisema kuwa, magari mawili yaliyokuwa yametegwa mabomu, yalilipuka karibu na ofisi ya kieneo katika mji wa Galkayo, katikati mwa nchi hiyo ambapo kwa akali watu 10 waliuawa na wengine watano kujeruhiwa. Aidha polisi imeripoti kujiri miripuko mingine miwili katika eneo la Mudug, lililoko kaskazini mwa Somali ambapo watu watano waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, baadhi wakiwa katika hali mahututi. Kundi la ash-Shabab limetangaza kuhusika na miripuko yote hiyo na kudai kwamba katika mashambulizi hayo kwa akali watu 30 waliuawa. Hii ni katika hali ambayo mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amelaani hujuma hizo. Taarifa iliyotolewa na ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNSOM) sanjari na kulaani mashambulizi yaliyotajwa, imetangaza kuwa kujiri matukio ya kigaidi wakati huu, kunaathiri mwenendo wa kuandaliwa uchaguzi wa bunge na rais nchini Somalia.

Francisco Caetano Jose Madeira, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Kabla ya hapo pia, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Afrika nchini humo alikuwa amesisitizia azma ya umoja huo ya kufanyika uchaguzi huo katika tarehe iliyopangwa. Kwa mujibu wa Francisco Caetano Jose Madeira, uchaguzi wa rais na bunge nchini Somalia utafanyika mwishoni mwa mwezi Septemba na mwanzoni mwa mwezi Oktoba kwa ushiriki wa taasisi zote za nchi hiyo. Afisa huyo wa Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa, kufanyika uchaguzi huo, si tu kwamba kutakuwa na mafanikio kwa Somalia pekee, bali kutahesabiwa kuwa ushindi kwa nchi zote za eneo na kimataifa. Kwa upande wake, Omar Mohamed Abdulle, mkuu wa tume ya uchaguzi ya Somalia ametangaza kuwa, uchaguzi wa rais utafanyika tarehe iliyopangwa yaani Oktoba 30.

Kampeni kuelekea uchaguzi wa rais na bunge nchini Somalia

Abdulle amewataka wanasiasa wote wa nchi hiyo na kadhalika jamii ya kimataifa kufanya juhudi kubwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika chini ya anga salama. Kwa mujibu wa Omar Mohamed Abdulle, tayari kumeundwa kikosi cha askari wa serikali ya Somalia kwa kushirikiana na wale wa AMISOM ambacho kitakuwa na jukumu la kusimamia usalama kwenye uchaguzi huo wa mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu.