Idadi ya wahanga wa shambulio la ash-Shabab mjini Mogadishu yaongezeka
Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab katika moja ya maeneo ya pwani mjini Mogadishu huko Somalia imeongezeka na kufikia 10.
Ali Abdullah, kamanda wa polisi mjini Mogadishu amesema kuwa, baada ya hujuma hiyo kulijiri mapigano ya kufyatuliana risasi ambayo yaliendelea hadi katikati ya usiku. Duru za polisi mjini Mogadishu zimeripoti kwamba, wanachama wa kundi hilo walitumia gari lililokuwa na mada za miripuko katika kushambulia hoteli moja mji hapo na kuanza kufyatua ovyo risasi.
Miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo ni raia sita na polisi wawili na wanachama wawili wa genge hilo.
Awali habari zilitangaza kuwa watu sita waliopoteza maisha katika tukio hilo. Jumapili iliyopita, kundi hilo la ash-Shabab lilifanya shambulizi kubwa mjini Mogadishu na kudai kuwa, kwa akali limeua watu 30 wakiwamo askari wa serikali .
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amelaani hujuma hizo. Taarifa iliyotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNSOM) imelaani mashambulizi hayo na kutangaza kuwa kujiri matukio ya kigaidi wakati huu, kunaathiri mwenendo wa kuandaliwa uchaguzi wa Bunge na Rais nchini Somalia.