Aug 28, 2016 14:16 UTC
  • Buhari: Kiongozi wa Boko Haram amejeruhiwa katika mashambulizi ya anga

Rais wa Nigeria ameeleza kuwa waasi wa eneo la Niger Delta na wanamgambo wa kundi la Boko Haram wanatambuliwa hivi sasa kuwa matishio mawili hatari.

Rais Muhammadu Buhari ambaye yupo ziarani Nairobi mji mkuu wa Kenya amethibitisha kuwa Abubakar Shekau kiongozi wa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram amejeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya jeshi na Nigeria.

Aidha amewatahadharisha waasi wanaobeba silaha katika eneo tajiri kwa mafuta la Niger Delta na kuongeza kuwa atakabiliana na waasi hao kama walivyofanywa wanamgambo wa kundi la Boko Haram.

Rais wa Nigeria ameyasema hayo leo pambizoni mwa  Kongamano la Sita la Kimataifa la Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) linalodhaminiwa na Japan jijini Nairobi Kenya. Hii ni katika hali ambayo hadi kufikia sasa makundi ya uasi yaliyoko Niger Delta hayajatoa radiamali yoyote kwa oparesheni mpya inayoendeshwa na jeshi la Nigeria.

Waasi wa Niger Delta eneo tajiri kwa mafuta nchini Nigeria

Buhari amebainisha kuwa kundi la Boko Haram linakaribia kusambaratika kufuatia kujeruhiwa kiongozi wa kundi hilo na kuongeza kuwa, hivi sasa limejibadilisha na kuwa vijikundi vidogo vidogo ambavyo havidhibiti tena eneo lolote lile.

Rais wa Nigeria amesema serikali ya nchi hiyo iko tayari kufanya mazungumzo na wanamgambo wa Boko Haram ili kuwaachia huru mabinti 218 waliowateka nyara katika mji wa Chibok.

Wakati huo huo Sani Othman Msemaji wa jeshi la Nigeria amekumbusha kuwa waasi wenye silaha wasiopungua watano wameuliwana wengine 23 kutiwa mbaroni katika operesheni ya karibuni iliyofanywa na jeshi huko Niger Delta.

Tags