Watuhumiwa saba wa ugaidi watiwa nguvuni Isiolo, Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14785-watuhumiwa_saba_wa_ugaidi_watiwa_nguvuni_isiolo_kenya
Jeshi la Polisi mjini Isiolo nchini Kenya linaendelea kuwasaili watu saba wanaoshikiliwa na jeshi hilo tangu wiki mbili zilizopita kwa tuhuma za kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la ash Shabab.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2016 23:46 UTC
  • Wanamgambo wa ash Shabab wa nchini Somalia
    Wanamgambo wa ash Shabab wa nchini Somalia

Jeshi la Polisi mjini Isiolo nchini Kenya linaendelea kuwasaili watu saba wanaoshikiliwa na jeshi hilo tangu wiki mbili zilizopita kwa tuhuma za kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la ash Shabab.

Gazeti la Daily Nation la nchini Kenya limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watuhumiwa hao ambao wana umri wa chini ya miaka 35, walitiwa mbaroni wakiwa na vitu ambavyo vinashukiwa kuwa ni vya masuala ya kigaidi kama vile kaseti zinachochochea misimamo mikali ya kidini. 

Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakikusanya watu mjini Isiolo ili wajiunge na kundi la ash Shabab. Wametiwa mbaroni mjini Isiolo katika siku na nyakati tofuati.

Gazeti hilo aidha limemnukuu Kamishna wa Kaunti ya Isiolo, Bw. George  Natembeya akisema jana kuwa, jeshi la polisi limeomba kupewa muda zaidi wa kuwasaili watuhumiwa hao kabla ya kuwapeleka mahakamani.

Mmoja wa watuhumiwa hao alikamatwa katika eneo la Bula Pesa kwa tuhuma za kuwaandalia safari ya Somalia vijana sita waliotoweka mwezi uliopita. Vijana watatu kati yao walikamatwa katika kambi ya wakimbizi ya Dagahaley, katika Kaunti ya Garissa mwezi uliopita wakati walipokuwa safarini kuelekea Somalia.

Kambi ya Wakimbizi ya Dadaab-Dagahaley Kaunti ya Garissa nchini Kenya

 

Taarifa zinasema kuwa, vijana hao walielekea Garissa kutoka Isiolo kwa kutumia pikipiki. Hadi hivi sasa vijana watatu wa eneo la Tullo Roba huko Isiolo hawajulikani walipo na inaaminiwa kuwa wako njiani kuelekea Somalia kujiunga na kundi la ash Shabab.