Al Shabaab washambulia Kenya, askari polisi wawili hawajulikani waliko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15859-al_shabaab_washambulia_kenya_askari_polisi_wawili_hawajulikani_waliko
Askari polisi wawili wa Kenya hawajulikani waliko kufuatia shambulio la kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabaab katika kituo cha polisi cha Kaunti ya Garissa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hayo yameelezwa na msemaji wa Polisi ya Kenya George Kinoti. 
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 22, 2016 11:09 UTC
  • Al Shabaab washambulia Kenya, askari polisi wawili hawajulikani waliko

Askari polisi wawili wa Kenya hawajulikani waliko kufuatia shambulio la kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabaab katika kituo cha polisi cha Kaunti ya Garissa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hayo yameelezwa na msemaji wa Polisi ya Kenya George Kinoti. 

Shambulio hilo ni la karibuni zaidi kufanywa na kundi hilo la kigaidi katika mlolongo wa mashambulio ya mpakani linayofanya ndani ya ardhi ya Kenya.

Taarifa ya Kinoti kuhusiana na shambulio hilo la usiku wa kuamkia leo imefafanua kuwa, washambuliaji waliokuwemo kwenye magari mawili aina ya Landcruisers walishambulia kituo hicho cha doria, lakini maafisa wa polisi waliweza kukabiliana nao katika ufyatulianaji mkali wa risasi.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi ya Kenya askari mmoja alijeruhiwa na wengine wawili hawajulikani waliko.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabaab limekiri kuhusika na shambulio hilo katika Kaunti ya Garissa. 

Msemaji wa Al-Shabaab Sheikh Abdiasis Abu Musab amevieleza vyombo vya habari kwa njia ya simu: "Tulishambulia kituo cha polisi jana usiku katika mji mdogo karibu na Garissa".

Dikteta wa Somalia Mohamed Siad Barre

Al-Shabaab limekuwa likishambulia mara kwa mara ndani ya ardhi ya Kenya likidai kuwa linafanya hivyo kujibu mapigo kwa hatua ya Kenya ya kutuma vikosi vyake nchini Somalia.

Kenya ilichukua hatua hiyo mwaka 2011 kukabiliana na upenyaji wa wanamgambo wa Al-Shabaab katika maeneo yenye usalama udhaifu ya mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Somalia.

Somalia imeharibiwa na vita vilivyoanza mwaka 1991 baada ya kuangushwa serikali ya dikteta wa nchi hiyo Mohamed Siad Barre. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabaab ambalo liliwahi kudhibiti karibu maeneo yote ya ardhi ya Somalia linataka kuiangusha serikali ya Rais Hassan Sheikh Mohamud inayoungwa mkono na madola ya Magharibi.../