UNHCR imewarejesha wakimbizi zaidi ya 30,000 wa Somalia kutoka Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16378-unhcr_imewarejesha_wakimbizi_zaidi_ya_30_000_wa_somalia_kutoka_kenya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema kuanzia mwezi Desemba mwaka 2014 wakimbizi zaidi ya elfu 30 wa Somalia wamerejeshwa kwa hiari katika nchi yao kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyoko kaskazini mashariki mwa Kenya.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Sep 30, 2016 04:26 UTC
  • UNHCR imewarejesha wakimbizi zaidi ya 30,000 wa Somalia kutoka Kenya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema kuanzia mwezi Desemba mwaka 2014 wakimbizi zaidi ya elfu 30 wa Somalia wamerejeshwa kwa hiari katika nchi yao kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyoko kaskazini mashariki mwa Kenya.

Katika ripoti iliyotolewa mjini Nairobi, UNHCR imesema katika mwaka 2016 pekee, wakimbizi 24,248 wamerejea Somalia kwa hiari ambapo katika wiki mbili za kwanza za mwezi huu wa Septemba wakimbizi 482 walirudi kwa ndege Somalia.

Kwa sasa Kenya inashirikiana na UNHCR katika mpango utakaohakikisha kurejeshwa kwa utaratibu na hiari wakimbizi 50,000 wa Somalia kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab, ambayo serikali ya Kenya ilitangaza kuifunga mapema mwaka huu.

Miezi kadhaa iliyopita serikali ya Kenya ilitangaza mpango wa kuifunga kambi ya Dadaab. Kambi hiyo inatazamiwa kufungwa kikamilifu kabla ya mwezi Mei mwaka 2017. Hata hivyo uamuzi huo na Kenya umekabiliwa na upinzani mkubwa huku viongozi mbalimbali wa nchi za eneo hilo na taasisi za kimataifa wakiitaka serikali ya Kenya kutupilia mbali uamuzi huo. Viongozi hao wanasema uamuzi huo wa Kenya wa kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni kinyume na sheria za kimataifa.

Pamoja na hayo yote, Kenya inaendelea kutilia mkazo uamuzi wa kufungwa kambi hiyo na tayari imeanzisha mchakato wa kuifunga baada ya kuundwa kamati ya pande tatu ya kushughulikia suala hilo.