Watu sita wauliwa na al Shabab nchini Kenya
Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la kigaidi la al Shabab wamewaua watu sita katika shambulio lililofanywa na kundi hilo leo asubuhi huko Kenya.
Kaunti ya Mandera inayopatikana katika mpaka na Somalia imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya kundi la al Shabab; ambalo linasema kuwa litaendeleza mashambulizi yake hayo huko Kenya hadi pale serikali ya Nairobi itakapoondoa wanajeshi wake huko Somalia. Kenya imetuma wanajeshi wake huko Somalia kama sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini humo.
Ali Roba Gavana wa kaunti ya Mandera ameeleza kuwa wamekumbwa na shambulio jingine la al Shabaab na kuthibitisha kuuliwa watu sita. Al Shabab wamefanya shambulio hilo leo asubuhi katika eneo kwa jina "Bulla Public Works".
Roba ameongeza kuwa hivi sasa wangekuwa wanazungumzia wahanga wengi wa shambulio hilo, lakini akasema askari usalama wa Kenya waliweza kutoa radiamali ya haraka dhidi ya al Shabab. Mashambulizi ya mara kwa mara ya wanamgambo wa al Shabab huko Kenya yamesababisha vifo vya mamia ya watu katika miaka mitatu iliyopita na pia kuathiri sekta muhimu ya utalii ya nchi hiyo.