Taarifa ya jumuiya ya SADC kuhusiana na kukabiliana na ukame
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16855-taarifa_ya_jumuiya_ya_sadc_kuhusiana_na_kukabiliana_na_ukame
Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC imetangaza kuwa, taathira za ukame kwa wananchi wa eneo la kusini mwa Afrika ni mbaya sana.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 06, 2016 13:25 UTC
  • Taarifa ya jumuiya ya SADC kuhusiana na kukabiliana na ukame

Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC imetangaza kuwa, taathira za ukame kwa wananchi wa eneo la kusini mwa Afrika ni mbaya sana.

Taarifa hiyo ya SADC imeeleza kwamba, nchi za ukanda huo zinahitajia kiasi cha dola bilioni mbili na milioni 200 ili ziweze kukabiliana na athari mbaya za ukame. Nchi za eneo la kusini mwa Afrika zinakabiliwa na hali mbaya kabisa ya ukame ambayo haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 35 iliyopita. Ukame mtawalia uliozikumba nchi za kusini mwa Afrika mwaka 2014 na 2015 na uhaba wa mvua uliotokea mwaka huu, umelifanya eneo hilo kukabiliwa na hali mbaya kabisa katika kipindi cha miaka 35 iliyopita.

Kati ya nchi hizo, Angola, Lesotho, Malawi, Botswana, Madagascar, Msumbiji na Zimbabwe zinakabiliwa na hali mbaya zaidi ya ukame ikilinganishwa na nchi nyingine. Katika baadhi ya maeneo ya nchi hizo visima na mito imekauka, mashamba yameteketea vibaya na mifugo inakufa kutokana na kukosa maji na malisho. Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuanzia sasa hadi Aprili mwaka ujao takribani dola bilioni moja na milioni mia mbili zinahitajika kwa ajili ya kudhamini misaada ya dharura kwa watu milioni 12 na mia tatu katika nchi saba ambao wanakabiliwa na hali mbaya mno iliyotokana na athari za ukame. Maisha ya raia hao hasa katika maeneo ya vijijini yameharibika mno na kupelekea kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu za chakula kama mahindi.

Hali ya ukame nchini Zimbabwe

Wataalamu wa masuala ya mazingira wanasema kuwa, ukame huo umetokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayojulikana kwa jina la El-Nino na hivyo kukwamisha mfumo wa kilimo katika nchi husika. Ukame huo umepelekea kuwa hatarini maisha ya wakazi wa eneo hilo. Aidha hali hiyo imekuwa na taathira hasi kwa uchumi wa nchi hizo. Nchi kama Zimbabwe na Malawi zinakabiliwa na hali mbaya zaidi ya umasikini kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo. Nchini Zimbabwe serikali ya nchi hiyo imeshindwa hata kuwalipa mishahara ya wafanyakazi na kuifanya nchi hiyo kukabiliwa na wimbi la maandamano na malalamiko ya wananchi.

Mwezi Juni mwaka huu Jumuiya ya SADC ilitoa wito wa kukusanywa dola bilioni mbili na milioni mia saba kwa ajili ya kukabiliana na ukame, lakini hadi sasa ni dola milioni 590 tu ndizo ambazo zimekusanywa hadi sasa. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika SADC ambayo ni asasi ya kiuchumi, inapaswa kuwa na nafasi amilifu zaidi katika suala zima la kupambana na ukame. 

Ukame na njaa unaoshuhudiwa barani Afrika sio mara ya kwanza kushuhudiwa katika bara hilo. Katika mazingira kama haya, wito wa SADC kwa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na ukame sio njia pekee ya kukabiliana na janga hilo la kimaumbile. 

Kutokana na ulimwengu hii leo kukabiliwa na migogoro mingi, nchi nyingi zinazokabiliwa na vita na machafuko barani Afrika zimesahauliwa. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuweko ushirikiano  wa kieneo barani Afrika, kutakuwa na taathira chanya katika kupunguza majanga ya kimaumbile barani humo kama janga la ukame.