Gavana wa Mombasa adai Masheikhe 24 wameuawa na serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17026-gavana_wa_mombasa_adai_masheikhe_24_wameuawa_na_serikali
Gavana wa ODM katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya ameikosoa vikali serikali kutokana na kukithiri mauaji ya washukiwa mbali mbali na hususan wa ugaidi na kudai kuwa vyombo vya usalama nchini humo vimeua Masheikh zaidi ya 24 katika miaka ya hivi karibuni.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Oct 08, 2016 23:32 UTC
  • Gavana wa Mombasa adai  Masheikhe 24  wameuawa na serikali

Gavana wa ODM katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya ameikosoa vikali serikali kutokana na kukithiri mauaji ya washukiwa mbali mbali na hususan wa ugaidi na kudai kuwa vyombo vya usalama nchini humo vimeua Masheikh zaidi ya 24 katika miaka ya hivi karibuni.

Naibu Kinara wa chama cha upinzani cha ODM, Hassan Joho ameituhumu serikali kuwa imekuwa ikitekeleza mauaji kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Akiashiria matukio ya hivi karibuni, Joho ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Mombasa, amesema hatima ya vijana 30  katika pwani ya Kenya haijulikani, baada ya maafisa wa polisi kuwaagiza wafike katika vituo vya polisi kwa ajili ya usaili na kuahidi kuwaachilia huru, lakini imekuwa ni kinyume na hivyo.

Mwanasiasa huyo wa upinzani amesema yumkini idadi ya vijana waliotoweka wakiwa mikononi mwa maafisa wa polisi nchini humo mwaka huu imepindukia 80, kinyume na ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Kutetea Haki za Binadamu.

Kadhalika Naibu Kinara wa ODM amedai kuwa serikali ya Jubilee imehusika katika mauaji ya hivi karibuni ya wanaharakati na wakosoaji wake, wakiwemo mfanyabiashara Jacob Juma, aliyekuwa mbunge wa Kabete George Muchai na wakili Willie Kimani.

Amina Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya

Hii ni katika hali ambayo, Ijumaa iliyopita, Balozi Amina Mohamed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya aliliambia shirika la habari la Aljazeera katika mahojiano kuwa, madai kuwa maofisa wa usalama nchini humo wanaua washukiwa wa uhalifu hayana ukweli wowote.