Misri yachukizwa na tahadhari iliyotolewa na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17041-misri_yachukizwa_na_tahadhari_iliyotolewa_na_marekani
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri imekosoa vikali tahadhari ya kiusalama iliyotolewa na Marekani kwa raia wake wanaoishi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2016 01:14 UTC
  • Misri yachukizwa na tahadhari iliyotolewa na Marekani

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri imekosoa vikali tahadhari ya kiusalama iliyotolewa na Marekani kwa raia wake wanaoishi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Wizara hiyo imesema tahadhari ya kutotembelea maeneo ya umma iliyotolewa na ubalozi wa Marekani mjini Cairo inaibua maswali mengi kuliko majibu na kwamba Misri haielewi ni kwa nini Washington imetoa tahadhari hiyo ya kiusalama bila kushauriana nayo na kutoa ufafanuzi.

Hivi karibuni ubalozi wa Marekani nchini Misri uliwataka Wamarekani wanaoishi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wajiepusha na mijumuiko mikubwa, kumbi za burudani, maduka na majengo ya biashara pamoja na viwanja vya michezo katika mji mkuu Cairo kuanzia Alkhamisi hadi Jumapili. Hata hivyo taarifa ya ubalozi wa Marekani mjini Cairo haikutoa ufafanuzi zaidi kuhusu tahadhari hiyo ya kiusalama.

Ubalozi wa Marekani mjini Cairo

Misri imesema tahadhari za aina hiyo hazifai na zinaweza kuwa na taathira hasi hususan kwa sekta ya utalii na uchumi wa nchi hiyo ya Kiafrika huku ikizitadharisha balozi zingine za nchi za nje nchini humo kujiepusha nazo.

Hii ni katika hali ambayo, balozi za Uingereza na Canada mjini Cairo pia zimewatahadraisha raia wao nchni Misri dhidi ya kutembelea maeneo ya umma yenye mikusanyiko mikubwa hadi Jumapili jioni.