Msafara wa polisi wa Misri washambuliwa kwa bomu
Polisi mmoja ameuawa na watu wengine 11 wamejeruhiwa baada ya kutokea mripuko katika msafara wa polisi hao kwenye mji wa al Arish nchini Misri.
Mtandao wa habari wa al Yaum as Sabi'i umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mripuko huo umetokea jana usiku kaskazini mwa jangwa la Sinai na kupelekea polisi mmoja kuuawa na watu wengine 11 kujeruhiwa, wanne kati yao wakiwa ni maafisa wa polisi.
Hadi hivi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mripuko huo.
Tangu mwaka 2013 wakati alipopinduliwa na jeshi Muhammad Morsi, Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri hadi hivi sasa, jeshi la nchi hiyo limekuwa likipambana na mashambulio mbalimbali hususan katika Rasi ya Sinai ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Machafuko yaliyozuka tangu mwaka 2013 hadi hivi sasa yameshapelekea mamia ya wanajeshi na polisi wa Misri kuuawa na kujeruhiwa.
Jenerali Abdul Fattah el Sisi aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'oa madarakani Mohammad Morsi na baadaye kuwa Rais wa Misri amesema kuwa, kundi la kigaidi lenye mfungamano na Daesh ni hatari kwa nchi hiyo na kwa nchi jirani.