Vikosi vya radiamali ya haraka vya Ufaransa kubaki CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18271-vikosi_vya_radiamali_ya_haraka_vya_ufaransa_kubaki_car
Ufaransa imesema kuwa wanajeshi wake wa radiamali ya haraka wataendelea kubakia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 27, 2016 10:52 UTC
  • Vikosi vya radiamali ya haraka vya Ufaransa kubaki CAR

Ufaransa imesema kuwa wanajeshi wake wa radiamali ya haraka wataendelea kubakia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema baada ya kikao cha baraza la ulinzi la nchi hiyo kuwa, muda wa kuhudumu wanajeshi wa radiamali ya haraka wa nchi  hiyo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati unamalizika mwezi Oktoba mwaka huu, lakini akasema kuwa vikosi hivyo vitaendelea kubakia nchini humo.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika mtaa mmoja wa mji mkuu wa CAR, Bangui

Hollande ameongeza kuwa vikosi vya radiamali ya haraka vya Ufaransa vitajiweka tayari kutekeleza oparesheni iwapo serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati itawasilisha ombi na kama kutakuwepo na tishio lolote kuu. Wanajeshi wa Ufaransa karibu 350 pamoja na ndege za nchi hiyo zisizo na rubani zitaendelea kubaki nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ufaransa ilituma wanajeshi wake 2000 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Disemba mwaka 2013 sambamba na kushtadi mgogoro wa ndani nchini humo. Rais Faustin Archange Touadera aliingia madarakani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Machi mwaka huu baada ya kuwepo serikali ya mpito chini ya uongozi wa Rais Catherine Samba Panza. Wananchi sasa wanataraji kuwa serikali na bunge jipya vitaweza kukomesha mapigano ya kidini na kikabila na hivyo amani ya kudumu kurejea nchini.