Waziri wa Awqaf Misri asisitiza kuhusu vita dhidi ya wenye misimamo mikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18349-waziri_wa_awqaf_misri_asisitiza_kuhusu_vita_dhidi_ya_wenye_misimamo_mikali
Waziri wa Awqaf nchini Misri amesisitiza kuhusu ulazima wa kukabiliana na misimamo mikali ya kidini sambamba na kuwepo jitihada za kueneza amani katika jamii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 28, 2016 23:08 UTC
  • Waziri wa Awqaf Misri asisitiza kuhusu vita dhidi ya wenye misimamo mikali

Waziri wa Awqaf nchini Misri amesisitiza kuhusu ulazima wa kukabiliana na misimamo mikali ya kidini sambamba na kuwepo jitihada za kueneza amani katika jamii.

Sheikh Mohamed Mokhtar Gomaa Waziri wa Awqaf nchini Misri ameyasema hayo mjini Cairo katika mkutano ulioitishwa kujadili maudhui ya kukabiliana na ugaidi na fikra za ukufurishaji.

Sheikh Gomaa ametoa wito kwa maulamaa na wanafikra wa Kiislamu kuandaa vikao na darsa katika vituo vya kidini kwa lengo la kuwaelimisha Waislamu kuhusu masuala ya ubinadamu na kupambana na misimamo mikali ya kidini.

Waziri wa Awqaf nchini Misri amesema kuna ulazima wa kukabiliana na wale wenye misimamo mikali ya kidini na wakati huo huo kueneza moyo wa urafiki, upendo na kuishi maisha ya amani na maelewano baina ya watu wote katika jamii.

Magaidi wakufurishaji wa Al Shabab wanaotekeleza hujuma Kenya na Somalia

Aidha Sheikh Gomaa amesema magaidi wanaeneza fikra potofu kwa lengo la kubadilisha utambulisho wa Waislamu duniani. Ameongeza kuwa, Wizara ya Awqaf nchini Misri inajitahidi kueneza fikra za misimamo ya wastani katika jamii na kwamba mojawapo ya njia zinazotumiwa kufikia lengo hilo ni kuanzisha misafara ya kidini inayotumwa katika maeneo mbali mbali ambapo Waislamu wanahimizwa kuhifadhi Qur'ani na kufungamana na maadili mema.