Watu 10 wauawa kaskazini mwa Misri
-
Wanajeshi wa Misri wakiwa katika operesheni ya kupambana na magaidi kaskazini mwa nchi hiyo
Watu 10 wameuawa katika mapigano baina ya jeshi la Misri na watu wenye silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Muhammad Samir, msemaji wa jeshi la Misri ametangaza habari hiyo leo Jumapili na kuongeza kuwa, watu sita wenye silaha na wanajeshi wanne wa serikali wameuawa katika mapigano hayo.
Amesema, wanajeshi wa Misri wamefanya mashambulizi dhidi ya makundi yenye silaha kaskazini mwa Rasi ya Sinai kwa lengo la kudhibiti usalama wa miji na vijiji vya eneo hilo kama vile miji ya al Arish, Rafah na Sheikh Zaid. Magaidi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye maeneo hayo. Polisi mmoja aliuawa jana na wengine wanne kujeruhiwa baada ya kuripukiwa na bomu katika mji wa Sheikh Zaid.
Tangu miaka miwili nyuma hadi hivi sasa, watu wenye silaha wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya viongozi na maafisa wa kulinda usalama pamoja na vituo vya kijeshi na vya polisi katika mkoa wa Sinai Kaskazini na kuua makumi ya watu na kujeruhiwa wengine kadhaa.
Mwezi Oktoba mwaka huu, jeshi la Misri lilifanya mashambulizi makubwa kwa ajili ya kuyafurusha magenge ya kigaidi katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Kuna makundi kadhaa ya kigaidi yanayofanya mashambulizi katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri na kundi kubwa zaidi ni lile linalojiita Answar Baytul Muqaddas ambalo mwezi Novemba 2014 lilitangaza utiifu kwake kwa genge la kitakfiri la Daesh na kujiita Wilaya ya Sinai.