Tanzania na Kenya zakubaliana kujenga barabara mbili unganishi
Tanzania na Kenya zimekubaliana kuanza kwa wakati ujenzi wa barabara mbili unganishi ambazo zitaboresha usafirishaji wa bidhaa na safari za raia kati ya nchi mbili hizo.
Makubaliano hayo yalifikiwa jana katika mazungumzo ya marais hao wawili na kutangazwa rasmi katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari jijini Nairobi. Makubaliano hayo yanamaanisha kuwa nchi mbili za Kenya na Tanzania hivi sasa zitaendelea mbele na majadiliano ili kufikia mchakato wa mwisho ambao utaipelekea Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kufadhili ujenzi wa barabara hizo kuu za Bagamoyo Malindi na ile ya kupitia mpaka wa Isebania katika kaunti ya Migori kuelekea Tanzania. Rais Uhuru Kenyatta amesema katika mkutano huo na mgeni wake Rais wa Tanzania kuwa, wana mpango wa kuhakikisha kuwa wanaharakisha ujenzi wa barabara hiyo kutoka Bagamoyo hadi Malindi na nyingine inayopitia Isebania ili kufungua ukanda wa magharibi na kuwawezesha watu kusafiri kwa usalama na kwa gharama nafuu. Rais John Magufuli jana alianza ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Kenya.