Nov 23, 2016 08:08 UTC
  • Hukumu ya miaka 2 jela kwa aliyenajisi mabinti 100 Malawi yakosolewa

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na asasi za kupambana na maambukizi ya virusi vya HIV nchini Malawi zimekosoa vikali hukumu ya kufungwa miaka miwili jela, iliyotolewa na mahakama moja nchini humo, dhidi ya mwathirika wa virusi vya HIV aliyewanajisi mabinti wadogo zaidi 100 kwa madai ya kuwasafisha na kuwafanyia tambiko la kimila na kiutamaduni.

Michael Chipeta, wakili na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini humo amekosoa hukumu hiyo na kusema kuwa kulikuwa na mapungufu mengi katika mchakato mzima wa kesi na hukumu dhidi ya mwathirika huyo wa virusi vya HIV, anayejulikana kama Eric Aniva mwenye umri wa miaka 45.

Rais Peter Mutharika wa Malawi

Naye Maziko Matemba, Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Health and Rights Education Program ameeleza kusikitishwa kwake na hukumu hiyo na kusisitiza kuwa, jitihada nyingi zinafaa kufanyika nchini humo kwa kuwahusisha wadau wote, ili kupunguza au kuzima maambukizi ya virusi vya HIV na ugonjwa hatari wa Ukimwi, haswa ikizingatiwa kuwa Malawi ni moja ya nchi zenye viwango vya juu vya maambukizi ya HIV duniani.

Eric Aniva  wa wilaya ya Nsanje alikiri kwamba amefanya ngono na wasichana wadogo kwa kulipwa fedha ambazo ni sawa na kati ya dola nne na saba za Marekani kwa kumbikiri kila mtoto mmoja, kwa imani kuwa ubikira ni mkosi na kwamba kitendo hicho kinawasafisha watoto hao pamoja na jamii hiyo.

Malawi ni katika nchi zenye maambukizi makubwa ya virusi vya HIV/Ukimwi duniani

Baada ya shirika la habari la BBC kuangazia utamaduni huo uliopitwa na wakati nchini Malawi, Rais Peter Mutharika wa nchi hiyo alitoa agizo la kukamatwa mtu huyo mwezi Julai mwaka huu.

Tags