Nov 27, 2016 15:46 UTC
  • Watu 30 wauawa na waasi mashariki mwa Kongo DR

Watu wasiopungua 30 wameuawa katika mapigano kati ya makundi mawili ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Joy Bokele, mkuu wa eneo la Lubero la mkoa wa Kivu Kaskazini amethibitisha kutokea mapigano makali mapema leo Jumapili kati ya makundi hasimu ya waasi ya Mai Mai Mazembe na Nande katika kijiji cha Luhanga na kusababisha mauaji hayo.

Ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, idadi ya watu waliouawa katika ghasia hizo ni 30 na waliojeruhiwa ni 20, aghlabu yao wakiwa wa kabila wa Kihutu.

Eneo la Lubero, Kivu Kaskazini

Mkuu wa eneo la Lubero mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa Kongo amesema vyombo vya usalama havijatambua lengo la mapigano hayo lakini shirika la kijamii la Study for the Promotion of Peace, Democracy and Human Rights limesema kundi la waasi la Nande limekuwa likitoa vitisho vya kuwashambulia Wahutu wa eneo hilo, kwa muda wa wiki moja.

Maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia machafuko na mapigano ya mara kwa mara kwa zaidi ya miaka 20 sasa. 

Kushindwa jeshi la nchi hiyo pamoja na askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa kuwamaliza wanamgambo wenye silaha kumepelekea kuongezeka machafuko na ukosefu wa utulivu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.

Tags