Al Azhar yasisitiza kulindwa vijana mkabala wa fikra potofu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20983-al_azhar_yasisitiza_kulindwa_vijana_mkabala_wa_fikra_potofu
Naibu wa Sheikhul Azhar wa Misri amewataka maulamaa wa Kiislamu wawaunge mkono zaidi vijana kukabiliana na hujuma za kifikra za maadui.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2016 23:39 UTC
  • Al Azhar yasisitiza kulindwa vijana mkabala wa fikra potofu

Naibu wa Sheikhul Azhar wa Misri amewataka maulamaa wa Kiislamu wawaunge mkono zaidi vijana kukabiliana na hujuma za kifikra za maadui.

Abbas Shuman, Naibu wa Sheikhul Azhar jana (Jumatano) alisema kuwa, kuwaunga mkono vijana ni moja ya majukumu muhimu ya maulamaa wa Kiislamu na hasa wa Al Azhar na kuongeza kuwa, maulamaa wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar wana nafasi muhimu katika kuwalinda vijana mbele ya hujuma za kifikra za mirengo ya kigaidi na ile yenye misimamo ya kufurutu ada. Abbas Shuman ameyasema mjini Cairo katika mkutano uliofanyika chini ya anwani "Vyombo vya Habari, Vijana na Fikra za Kidini zenye Malengo Maalumu." 

Abbas Shuman Naibu wa Sheikhul Azhar

Naibu wa Sheikul Azhar ameongeza kuwa, Chuo Kikuu cha Al Azhar kinaendesha mkutano huo na makongamano mbalimbali nje ya Cairo ili kujibu na kukabiliana na fikra potofu za maadui. Abbas Shuman ameashiria uungaji mkono wa Al Azhar kwa mazungumzo yoyote kati ya dini mbalimbali na kueleza kuwa mikutano na vikao vinavyoendeshwa na chuo hicho kikuu haviwahusu maulamaa wa chuo hicho pekee, bali watu wote wanaweza kushiriki kwenye mikutano hiyo.