Maafisa sita wa polisi wauawa katika hujuma ya kigaidi Cairo
Maafisa sita wa polisi nchini Misri wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa leo Ijumaa baada ya bomu la kutegwa barabarnai kulipuka katika kituo kimoja cha upekuzi mjini Cairo.
Hujuma hiyo ya kigaidi imejiri karibu na jengo la serikali katika barabara ya kuelekea katika eneo la kitalii la Piramidi za Giza.
Hakuna yeyote aliyedai kutekeleza hujuma hiyo ya kigaidi ambayo pia imepelekea kujeruhiwa raia wane. Usalama umeimarishwa katika eneo la mlipuko ambalo pia liko karibu na Msikiti katika mtaa huo wa Giza.
Shambulizi hilo limetajwa kuwa baya zaidi kujiri katika mji mkuu wa Misri katika miezi ya hivi karibuni.
Maafisa wa usalama Misri pia wamekuwa wakidai kuwa Harakati ya Ikhwanul Muslimin inahusika na ugaidi. Mwanachama wa Ikhwanul Muslimin Muhammad Mursi aliyetawala Misri kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kupinduliwa na jeshi Julai 2013 pia anashikiliwa kwa tuhuma za ugaidi.
Harakati ya Ikhwanul Muslimina ya Misri imekanusha madai kuwa chama hicho kinashirikiana na makundi ya kigaidi.
Mamia ya polisi na wanajeshi wa Misri wameuawa katika uasi unaoendelezwa na kundi la kigaidi la Daesh au ISIS hasa katika eneo la Rasi ya Sinai.