Mchanganuzi: US, UK na Israel zimezitelekeza Sudan mbili baada ya kuzitenganisha
Katika hali ambayo Sudan Kusini inatimiza miaka mitatu ya mapigano, machafuko na uhasama, wachanganuzi wa mambo wanasema kuwa, Marekani, Uingereza na Israel zimeitelekeza nchi hiyo na jirani yake Sudan, licha ya kuhusika moja kwa moja katika mpango wa kuzitenganisha.
Abayomi Azikiwe, Mhariri wa shirika la habari la Pan-African News Wire, ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa amesema serikali za Washington, London na Tel Aviv ndizo zilizoshinikiza kutengana nchi mbili hizo mwaka 2011, kutokana na uchu na tamaa ya kutaka kustafidi na utajiri wake wa mafuta.
Amesema licha ya kushinikiza kutengana nchi mbili hizo, Marekani, Uingereza na utawala haramu wa Israel hazishughulikii ipasavyo mgogoro wa kiusalama na kisiasa unaoikabili Sudan Kusini kwa sasa.
Abayomi Azikiwe, Mhariri wa Pan-African News Wire amefafanua kuwa, lengo la tawala tatu hizo za kibeberu kuzitenganisha Sudan ni kutaka kudhibiti rasilimali na utajiri wake wa mafuta, baada ya kuona kuwa nchi hiyo ilikuwa inaelekea kuwa moja ya nchi zinazozalisha kwa wingi bidhaa hiyo muhimu duniani, haswa kutokana na namna ilivyokuwa imekwea katika soka la mafuta duniani ndani ya muongo mmoja uliopita.
Sudan Kusini ijitenga na Sudan Julai mwaka 2011 na kujikuta katika vita vya ndani Disemba mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua madarakani.
Akihutubia bunge hapo jana Jumatano, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alitoa wito wa kufanyika 'Mazungumzo ya Kitaifa' ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa na kiusalama unaoikabili nchi hiyo kwa muda wa miaka mitatu sasa.
Hii ni katika hali ambayo, Afrika Kusini imethibitisha kuwa, kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar amepewa kifungu cha nyumbani ili kumzuia kuondoka nchini humo. Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa, Machar ataendelea kuwa nyumbani kwake jijini Pretoria na kwamba mawasiliano yake ya simu yatafuatiliwa.