Sudan yaongeza muda wa usitishaji vita katika maeneo yenye mzozo
Rais wa Sudan ametangaza kuongeza muda wa usitishaji vita kwa mwezi mmoja mwingine katika maeneo yanayozozaniwa nchini humo.
Rais Omar al Bashir wa Sudan amezitaka pande zinazopinga mazungumzo ya kitaifa nchini humo kukubali hati ya kitaifa ambayo ilipasishwa katika Mkutano wa mazungumzo ya kitaifa mwezi Oktoba mwaka jana. Rais Omar al Bashir ameyasema hayo kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 61 wa uhuru wa nchi hiyo. Rais wa Sudan amebainisha kuwa,hati ya kitaifa inazihusu pande zote na ni ya wananchi wote wa Sudan. Wakati huo huo Al Bashir kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, Sudan inaunga mkono kupatikana amani huko Sudan Kusini na kutekelezwa makubaliano yote yaliyosainiwa na nchi mbili hizo.
Mapigano yalianza katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan tangu mwaka 2003; ambapo makabila yenye silaha ya eneo hilo yaliituhumu serikali ya Khartoum kuwa baguzi. Mzozo katika eneo hilo hadi sasa umesababisha kuuliwa watu laki tatu na kuwafanya wakimbizi wengine karibu milioni mbili na laki tano.