Jan 04, 2017 07:14 UTC
  • Ethiopia yawafunga jela wanaharakati wanaoshinikiza sheria za Kiislamu

Mahakama moja nchini Ethiopia imewahukumu vifungo jela wanaharakati 20 wa nchi hiyo ambao wamekuwa wakishinikiza kutumika sheria za Kiislamu nchini humo.

Mahakama hiyo imetumia sheria tata ya kupambana na ugaidi kuwahukumu vifungo jela wanaharakati hao wakiwemo waandishi wa habari wawili wanaofanya kazi katika kituo kimoja cha redio cha Kiislamu.

Shirika la habari lenye mfungamano na serikali la Fana Broadcasting Corporate limetangaza kuwa, wanaharakati hao wamehukumiwa kifungo cha miaka mitano na nusu jela kila mmoja kwa kupatikana na hatia ya kujihusisha na harakati inayochochea ghasia na kuhatarisha usalama wa taifa.

Maafisa usalama wakikabiliana na waandamanaji nchini Ethiopia

Wakili wa wanaharakati hao wa Kiislamu, Mustafa Safi, amesema wateja wake hawakutendewa haki katika kesi dhidi yao na kusisitiza kuwa atakata rufaa kupinga hukumu hizo.

Waislamu wa Ethiopia wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara ya kuishinikiza serikali ikomeshe dhulma na ubaguzi dhidi yao tangu mwaka 2011.

Hivi karibuni shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa wito wa kusitishwa ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Ethiopia dhidi ya raia na wakosoaji wa serikali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags