Wabunge wa Uganda watuma faili la mauaji ya Kasese ICC
Kundi la wabunge wa Uganda limetuma ombi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, likiitaka ianzishe uchunguzi juu ya mauaji yanayodaiwa kufanywa na maafisa usalama katika mji wa Kasese, jimbo la Rwenzori mwishoni mwa mwaka uliopita 2016.
William Nzoghu, mbunge kutoka eneo la Rwenzori na mmoja wa wajumbe sita wa bunge la nchi hiyo ya Afrika Mashariki walioiandikia barua ICC amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, zaidi ya watu 200 waliuawa katika operesheni ya pamoja ya jeshi na polisi ya Uganda katika eneo hilo. Mbunge huyo amesisitizia udharura wa ICC kuzingatia ombi lao na kuanzisha uchunguzi mara moja kuhusu tuhuma hizo za mauaji na jinai dhidi ya binadamu.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC imethibitisha kwamba tayari imepokea barua ya wabunge hao wa Uganda na itatoa muelekeo na radiamali yake katika siku zijazo.
Takwimu rasmi zinasema kuwa, wafuasi karibu 50 wanaounga mkono mfumo wa kifalme nchini Uganda pamoja na maafisa 16 wa polisi waliuawa katika mapigano baina ya pande mbili hizo yaliyotokea mwezi Novemba 2016 kwenye mji wa Kasese katika mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Serikali ya Kampala kupitia Jeje Odongo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki alikanusha tuhuma zilizotolewa na Amnesty International kuwa askari wa serikali walifanya mauaji ya kiholela katika eneo hilo na kisha kufukia miili ya watu waliouawa.
Mfalme wa Rwenzururu eneo la Rwenzori, Charles Wesley Mumbere, ambaye kwa sasa anazuiliwa na vyombo vya usalama anakabiliwa na mashitaka kadhaa, yakiwemo ya mauaji na kuchochea machafuko mjini Kasese.